Niger patieni kipaumbele maslahi ya wanawake na watoto wa kike: Ban

6 Novemba 2013

Ujumbe wa ngazi ya juu unaoongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon huko Sahel umekuwepo Niger ambapo pamoja na mambo mengine umeangazia suala la kuwawezesha wanawake huku Benki ya dunia ikiongeza dau la usaidizi. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Ripoti ya Joshua)

Siku ya tatu ziarani huko Ukanda wa Sahel, Bwana Ban na viongozi wa Benki ya dunia, Umoja wa Afrika na ule wa Ulaya walitia nanga mjini Niamey, Niger. Wamekuwa na mazungumzo na viongozi mbali mbali akiwemo Rais wa nchi hiyo Mahamadou Issoufou. Kubwa lililoangaziwa ni wanawake na watoto wa kike katika nchi ambayo bado suala hilo ni finyu. Bwana Ban akasema maamuzi yoyote yale yawe ya kisiasa, kiuchumi, kijamii lazima yazingatie kundi hilo muhimu kwa kuwa…

(Sauti ya Ban)

Tunapowapatia wanawake elimu iwafaayo, jamii inakuwa thabiti. Tukilinda haki za wanawake, jamii inakuwa na usawa. Na tunaporuhusu wanawke waamue hatma yao, basi watasongesha maendeleo kwa wote.”

Rais wa Benki ya dunia Jim Yong Kim akaunga mkono wito wa pamoja na Umoja wa Mataifa wa kuchukua hatua kwa afya na elimu kwa wanawake na watoto wa kike huko Sahel kwa kuahidi kuwekeza dola Milioni 200 kwenye mradi mpya wa kuboresha afya ya wajawazito na uzazi kwa watoto wa kike.