Harakati za kuleta maridhiano Juba, Kusini mwa Somalia zaendelea

5 Novemba 2013

Kundi la ngoma za kitamaduni likitumbuiza kwenye kusanyiko la viongozi wa serikali kuu, serikali ya mkoa na viongozi wa kidini na kikabila, mjini Mogadishu, Somalia, kubwa hapa ni mkutano wa maridhiano wa Juba, lengo ni kuongeza wigo wa uongozi wa serikali kuu kwenye eneo hilo na kudhibiti migongano baina ya koo. 

Wajumbe wako makini kwenye kikao hiki kinachofuatia kile cha IGAD kilichofanyika Ethiopia mwezi Agosti mwaka huu kujenga uhusiano mwema kati ya serikali na mamlaka ya Juba kusini mwaSomalia. Waziri Mkuu wa Somalia Abdi Farah Shirdon..

  “ Tunataraji kubeba jukumu kubwa katika kuwezesha mamlaka hii ya muda ili iweze kutekeleza kazi zake za utawala Juba na kuunganisha eneo lote la Juba ndani ya kipindi cha miaka miwili au chini ya hapo iwapo jitihada zaidi zitachukuliwa kufanikisha hilo.”

 Mkuu wa mamlaka ya muda huko Juba Sheikh Ahmed Mohamed akafunguka..

  “Hebu tuwe na sauti moja, na lengo moja. Hebu tusahau tofauti zetu na tuungane pamoja. Hebu tuangalie jambo zuri kwa kila mmoja wetu na tusahau fikra za chuki dhidi yetu. Hebu tuache kusema jambo moja na baadaye kulipinga.”

 Maridhiano haya yamekuwa yakipatiwa usaidizi na Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchiniSomalia, UNSOM na hapa Mkurugenzi wa utawala wa sheria Waldemar Very anasema…

  “Mafanikio ya mkutano huu yatavuka mipaka ya Juba. yataweka kasi na muundo wa jitihada za maridhiano kwa maeneo mengine ya Somalia.”

 Bila shaka kupatikana kwa amani kutachagiza amani na maendeleo huko Juba na utamaduni utatamalaki kuvuka mipaka..