Tumeshindwa kupanga tarehe ya mkutano wa pili wa Geneva: Brahimi

5 Novemba 2013

Matarajio ya kufanyika karibuni kwa mkutano wa pili wa Geneva kuhusu Syria hayakuweza kutimia hata baada ya msururu wa mikutano ya leo, amesema mjumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za kiarabu Lakhdar Brahimi mjini Geneva hii leo alipozungumza na waandishi wa habari. Bwana Brahimi katika mazungumzo ya pande tatu yakihusisha Umoja wa Mataifa, Urusi na Marekani lengo lilikuwa maandalizi ya mkutano huo lakini wameshindwa kupanga tarehe ya karibuni…

(Sauti ya Brahimi)           

“Tulitumai kuwa tungaliweza kupanga tarehe ya mkutano wa pili hii leo, lakini kwa bahati mbaya hatuwezi. Tunahangaika kuona iwapo tunaweza kuwa na mkutano huo kabla ya mwisho wa mwaka. Tumekubaliana kukutana kwenye mkutao wa utatu tarehe 25 novemba na unavyofahamu Umoja wa Mataifa tuko tayari na Katibu Mkuu anashindwa kuvumilia.”

Bwana Brahimi amesema mzozo wa Syria unazidisha idadi ya wakimbizi wa ndani na nje ya nchi kila siku ambapo sasa kwa wastani watu Elfu Sita huondoka nchini  humo kila siku na kwamba misaada ya kibinadamu na kifedha haitakuwa na maana bali kumaliza mgogoro huo.

(Sauti ya Brahimi)

“Lakini kwa muda gani watu wataendelea kupatia Syria msaada wa dola Bilioni Tano kila baada ya miezi Sita? Suluhisho la sasa la janga la kibinadamu siyo endelevu! Suluhisho la ukweli ni lile la kisiasa kwenye mzozo huu.”

Kuhusu washiriki wakuu wa mkutano huo wa pili wa Genava, Bwana Brahimi amesema ni upande  wa serikali na wapinzani ambapo kwa sasa upande wa upinzani unaendelea na maandalizi.

Akiwa Geneva hii leo pia Bwana Brahimi alikuwa na mazungumzo na wawakilishi wa nchi Tano zenye ujumbe wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wawakilishi nchi jirani na Syria ambazo ni Uturuki, Iraq na Lebanon pamoj na  wawakilishi wa ICRC na mashirika ya usaidizi wa kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.