Hali inazidi kuwa mbaya Syria kila uchao: Mkuu wa OCHA

5 Novemba 2013

Naona hali inazidi kuwa mbaya kwa wananchi wa Syria iwapo suluhu la kisiasa halitapatikana, ni kauli ya Valerie Amos Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu aliyotoa wakati wa kikao kati yake na watendaji wa ofisi hiyo kutoka sehemu mbali mbali duniani. Kikao hicho kilifanyika New York na kuunganishwa na ofisi zaAbidjan,Cairo,Geneva,Kabul, DR Congo kwa njia ya Video. Bi. Amos amesema idadi ya wanaohitaji msaada ndani ya Syria imefikia Milioni Tisa na kutokana na mzozo unaoendelea kuna maeneo ambayo hawajaweza kufika kwa miezi mitatu sasa. Hivyo akasema…

(Sauti ya Valerie)

“Ninaona hali inazidi kuwa mbaya kwa wananchi wa Syria iwapo suluhu ya kisiasa haitapatikana karibuni. Hivyo sina habari njema vile ambavyo suala hili linaweza kupatiwa suluhu. Tunalazimika kupatia mzozo huu kipaumbele cha hali ya juu, na hili ni jambo tunalofanyiwa tathmini duniani, na ni ajenda ya kimataifa kwa sasa.”

Mkuu huyo wa OCHA amesema kando mwa Syria kuna maeneo mengine ambako watu wanahitaji pia msaada hivyo ni vyema mzozo huo ukapatiwa suluhu huku akitoa shukrani kwa watendaji wa OCHA kwa kujitoa kwa dhati kutekeleza majukumu yao. Bi Amos akatumia kikao hicho kutaarifu juu ya mkutano wa ngazi ya juu wa usaidizi wa kibinadamu.

(Sauti ya Valerie)

“Katibu Mkuu sasa ameridhia mkutano wa usaidizi wa kibinadamu utaofanyika mapema mwaka 2016 huko Istanbul. Utakuwa ni mkutano wa kwanza wa aina hiyo. Kwa mantiki hiyo utakuwa ni wa kipekee. Lakini ule mchakato wa kufanyika mkutano huo ni muhimu kuliko mkutano wenyewe.”