Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya boti kuzama huko Myanmar, makumi ya watu hawajulikani waliko: UNHCR

Baada ya boti kuzama huko Myanmar, makumi ya watu hawajulikani waliko: UNHCR

Huko Pwani ya Myanmar, majanga ya vifo vitokanavyo na safari za mashua yameendelea kuchukua kasi ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linataja Jumapili kuwa ni siku mbaya zaidi kwani makumi ya watu wakiwemo watoto na wanawake wanahofiwa kufariki dunia  baada ya mashua waliyokuwa wakisafiria kusaka maisha bora kuzama.

Msemaji wa UNHCR Adrian Edwards amesema watu 70 wanaosadikiwa kutoka eneo la Rohingya jimbo la Rakhine nchini Myanmar walikuwemo kwenye mashua hiyo na hadi sasa waliookolewa ni watu wanane pekee.

Shirika hilo lina hofu kuwa majanga kama yale yanayotokea kwenye bahari ya Mediterranean yanawezak kutokea huko Asia iwapo nchi husika hazitachukua hatua kushughulikia mambo yanayofanya mamia ya watu kuweka maisha yao hatarini baharini ili kusaka maisha bora ugenini. Watu 140,000 bado hawana makazi huko Rakhine kutokana na ghasia za kikabila zilizoanza mwezi Juni mwaka jana.

Edwards amesema idadi kubwa ya wakazi wa Rohingya hawana uraia wa Mynamar na hivyo kutokana na ugumu wa maisha huamua kufanya safari hizo za hatari na mara nyingi hutumbukia kwenye mtego wa wasafirishaji haramu wa binadamu.

UNHCR imesema iko tayari kusaidia serikali ya Myanmar kushughulikia chanzo cha mzozo ikiwemo utatuzi wa suala la wakazi wa Rohingya kutokuwa na utaifa.