Umoja wa Mataifa umejizatiti kusaidia Mali: Ban

5 Novemba 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon pamoja na viongozi wengine wa ngazi za juu wanaoambatana naye kwenye ziara huko ukanda wa Sahel wamekuwa na mazungumzo na Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali mjini Bamako kando ya mwa mkutano wa kikanda wa mawaziri unaofanyika mjini humo.

Katika mazungumzo yao Bwana Ban amerejelea mshikamano wake na wananchi na serikali ya Mali na amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto zinazokabili ukanda huo.

Amekaribisha mkutano huo wa mawaziri ulioandaliwa na serikali ya Mali kama fursa ya kusikiliza tashwishwi na vipaumbele vya nchi za eneo hilo.

Bwana Ban na Rais Keita pia wamejadili hali ilivyo nchii Mali ambapo Katibu Mkuu amesifu maendeleo yalopatikana baada ya makubaliano ya Ouagadougou yaliyowezesha kufanyika kwa uchaguzi wa Rais.

Amesema anatambua kuwa uchaguzi huo ulikuwa ni hatua ya awali ya kuleta utulivu na amani na kusisitiza umuhimu wa kushughulikia chanzo cha mzozo unaoendelea ikiwemo kupatia suluhu suala la utawala bora, ulinzi wa haki za binadamu na kupanua wigo wa uongozi wa serikali kuu nchini humo.

Amemhakikishia Rais Keita azma yake ya kuimarisha uwezo wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA ili uweze kutekeleza mamlaka yake.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter