Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taarifa za kusitisha uhasama DR Congo zatia matumaini: Wajumbe

Taarifa za kusitisha uhasama DR Congo zatia matumaini: Wajumbe

Kundi la wajumbe maalum wakiongozwa na Umoja wa Mataifa Jumatatu wamesema wanazingatia taarifa za kusitisha uhasama kati ya waasi wa M23 na serikali ya DR Congo na kutaka waasi hao kuachana na uasi kama ilivyokubali awali. Taarifa ya pamoja wajumbe hao wakiongozwa na yule wa Maziwa Makuu Mary Robinson wamesema wana hofu juu ya kuibuka tena kwa mapigano lakini kutangazwa kwa kusitisha uhasama ni hatua ya kwanza na muhimu kwa ajili ya amani na hivyo wameitaka pia serikali ya DR Congo kujizuia wakati huu kufanya mashambulizi zaidi wakati huu. Wajumbe wengine ni mkuu wa MONUSCO Martin Kobler, mjumbe wa Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na Marekani

Mazungumzo kati ya M23 na serikali ya DR Congo yanafanyika Kampala, chini ya uratibu wa mwenyekiti wa mkutano wa kimataifa wa Maziwa Makuu Rais Yoweri Museveni wa Uganda kama msuluhishi na Waziri wa ulinzi wa Uganda Crispus Kiyonga akiwa ni mwezeshaji.

Wakati hayo yakiendelea, Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma anaendesha kikao cha Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC mjini Pretoria, ukihusisha pia ujumbe kutoka DR Congo.

Akizungumzia vikao hivyo vya Maziwa Makuu na SADC, Bi. Robinson na wajumbe wengine maalum huko DR Congo wamesema ni fursa nzuri y a kujenga maafikiano ili kumaliza mkwamo na mzozo na hatimaye kutekeleza mpango wa amani, ulinzi na ushirikiano wa eneo hilo uliotiwa saini mwezi Februari mwaka huu huko Addis Ababa, Ethiopia.