Baraza la Usalama lalaani mauaji ya waandishi wa habari nchini Mali

3 Novemba 2013

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali utekaji nyara na mauaji ya waandishi habari wawili Wafaransa katika eneo la Kidal nchini Mali, mnamo Novemba 2, 2013. Wanachama hao wa Baraza la Usalama wametuma risala za rambi rambi kwa familia za wahanga, pamoja na serikali ya Ufaransa. Wamesema, kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, waandishi wa habari na watu wengine wanaotoa huduma zenye hatari za kitaaluma katika maeneo ya migogoro huchukuliwa kama raia, na wanatakiwa kuheshimiwa na kulindwa kama raia. Wanachama hao wa Baraza la Usalama pia wametoa kumbusho la kutaka pande zote zinazohusika katika migogoro kuwajibika ipasavyo chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, na kusisitiza kuwa walohusika katika mauaji hayo ya waandishi wa habari watawajibishwa kisheria. Wametoa wito pia kwa serikali ya Mali kufanya uchunguzi haraka na kuwafikisha wahalifu hao mbele ya vyombo vya sheria, huku wakizingatia kuwa vitendo vyovyote vya kigaidi ni uhalifu usokubalika, bila kujali kinachouchochea, mahali unapofanyika, wakati na mtu anayeutekeleza. Wamerejelea ahadi yao ya kuunga kikamilifu ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA, na vikosi vya Ufaransa vinavyousaidia ujumbe huo, na kutaka pande zote zinazozozana kushirikiana na ujumbe wa MINUSMA.

.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter