Hali Mashariki mwa DRC imedhibitiwa lakini bado kuna makundi ya waasi: MONUSCO

1 Novemba 2013

Hali katika Kivu ya Kaskazini imedhibitiwa sasa, ingawa kundi la waasi wa M23 bado lina himaya katika miji miwili midogo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Hayo yamesemwa na Jenerali Santos Cruz, kamanda wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kuweka utulivu katika DRC, MONUSCO.

Katika mahojiano na Redio ya Umoja wa Mataifa, Jenerali Cruz amesema ingawa haiwezi kusemekana kuwa waasi wa M23 wameshindwa kijeshi, ufanisi ulopatikana na jeshi ya serikali ya DRC likisaidiwa na MONUSCO ni muhimu mno, na hali imebadilika kwa kiasi kikubwa kutoka ilivyokuwa wiki ilopita.

Ameongeza kuwa kuna makundi mengine mengi ya waasi, na MONUSCO hailengi tu kuchukuwa hatua za kijeshi dhidi ya M23 pekee, ila makundi hayo yote ya waasi.

“Tunajikita katika kusaidia DRC kuwalinda raia katika njia tofauti. Tunashiriki katika hatua za kijeshi, na sina shaka kuwa tutapata ufanisi katika majukumu yote tuliyopewa na Baraza la Usalama.”

Kuhusu uwezo wa jeshi la DRC kudhibiti hali bila usaidizi wa MONUSCO, Jenerali Cruz amesema hali inaendelea kuimarika kila siku.

“Ni dhahiri kuwa FARDC, yaani jeshi la DRC, limefanya vizuri sana. Wanapigana na makundi ya silaha, wanajaribu wawezavyo kuleta amani katika eneo hili la nchi, na tunawasaidia, kwa sababu ni jukumu letu, na ni rahisi kuona kuwa wanazidi kuimarika, na ni matumaini yetu kuwa kila siku tuendelea kutenda vizuri zaidi katika kutimiza majukumu yetu.”