Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAIDS yaonya kuhusu mzigo wa HIV uzeeni

UNAIDS yaonya kuhusu mzigo wa HIV uzeeni

Visa vya HIV na UKIMWI miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 50 na zaidi vinazidi kuongezeka kote duniani, kulingana na utafiti mpya ulofanywa na Shirika linalohusika na HIV na UKIMWI katika Umoja wa Mataifa, UNAIDS. Taarifa kamili na Alice Kariuki

(TAARIFA YA ALICE KARIUKI)

Utafiti huo umebinisha kuwa, watu milioni 3.6 wenye umri zaidi ya miaka 50 wanaishi na virusi vya HIV, wengi wao, wapatao milioni 2.9 wakipatikana katika nchi zinazoendelea.

UNAIDS imesema takriban watu laki moja wenye umri wa zaidi ya miaka 50 wanaambukizwa virusi vya HIV kila mwaka, kupitia mienendo hatari inayopatikana miongoni mwa vijana, kama vile kufanya mapenzi yaso salama na madawa ya kulevya.

UNAIDS imetoa wito wa kuongeza juhudi za kuzuia maambukizi ya HIV miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 50 na zaidi, ikiongeza kuwa hatari ya wao kufa ipo juu zaidi ya ile ya vijana, kwa sababu za matatizo mengine ya kiafya uzeeni.Peter Ghys, ni mkuu wa takwimu katika UNAIDS

Tunapendekeza uwepo uzingativu mahsusi kwa mahitaji ya kundi hili la watu, nah ii ni katika mambo machache. Kwanza, kuhakikisha kuwa kampeni zote za kuhamasisha na programu za kuzuia maambukizi zinawalenga watu hawa. Matibabu pia yaanze mapema kwa watu wa umri wa miaka 50 na zaidi, kwani uhai wa watu wote wanaopata matibabu hurefushwa, lakini watu wazee wamo hatarini zaidi, na uhai wao huwa mfupi kidogo kwa kulinganisha. Mwisho, ni kwamba huduma za afya kwa watu hawa zijumuishe matatizo mengine yote ya afya yatakayohitaji kutibiwa.”

Kwa mujibu wa UNAIDS, takriban watu milioni 35 wanaishi na virusi vya HIV kote duniani.