Mshikamano wa kimataifa uwe kitovu cha ajenda ya baada ya 2015: Mtaalamu

1 Novemba 2013

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu na mshikamano wa kimataifa Virginia Dandan, ametaka nchi wanachama wa Umoja huo kuweka mbele mshikamano wa kimataifa kama msingi wa mafanikio ya ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015.

Katika ripoti yake kwa Baraza la Kuu mjini New York, Dandan amesema kupitia mshikamano wa kimataifa watu wanakuwa na uhuru wa kufurahia manufaa ya jamii ya kimataifa inayoishi pamoja kwa amani ambapo pia haki za binadamu na uhuru vinazingatiwa.

Bi. Dandan pia aliwasilisha rasimu ya azimio kuhusu haki za watu kwa mshikamano wa kimataifa, rasimu ambayo itawasilishwa kwenye kikao cha  26 cha baraza la haki za binadamu mwezi Juni mwakani. Akizungumzia rasimu hiyo, amesema ni muhimu katika kusongesha harakati za kutambua haki za binadamu kwa mshikamano wa kimataifa na kwamba kwa kupitisha azimio hilo nchi zitaunda chombo cha kushughulikia changamoto kuu za haki za binadamu kama vile umaskini na ukosefu wa usawa.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter