Wakimbizi wa Angola waliokuwa Botswana warejea makwao

1 Novemba 2013

Kundi la mwisho la wakimbizi wa Angola nchini Botswana limeondoka jana hii ikiashiria kufungwa rasmi kwa kambi hiyo kongwe barani Afrika.Kundi la wakimbizi hao ambao walikuwa wakiishi katika kambi ya Dukwi waliwasili jana mchana katika eneo la Mashariki mwa Angola wakiwa na mafurushi yao. Taarifa na George Njogopa

(Taarifa ya George)

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR lilitangaza kufungwa kwa kambi hiyo kuanzia Octoba 30 ikiwa imepita miezi miwili tangu serikali ya Botswana kutangaza kufuta hadhi ya ukimbizi kutokana na maridhiano yaliyofikiwa hapo yaliyotoa fursa kwa wakimbizi hao kurejea kwenye maeneo yao ya asili.

Vita vya kupigania uhuru nchini Angola vilivyodumu kuanzia mwaka 1961 mpaka 1975 na baadaye kuzuka kwa machafuko ya kiraia ya mwaka 1975 mpaka 2002 ni matukio yaliyozalisha idadi kubwa ya wakimbizi katika mataifa ya jirani.

Vita hivyo pamoja na machafuko ya kisiasa ilisababisha maelfu ya raia kupoteza maisha na wengine zaidi ya milioni 4 walikimbilia katika mataifa ya jirani ikiwemo watu 555,000 ambao walitambuliwa kama wakimbizi.

Idadi kubwa ya raia walikimbilia katika mataifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Zambia, Namibia, Afrika Kusini na Botswana. Kurejea nyumbani kwa wakimbizi hao waliosalia huko Botswana kunafungua ukurasa mpya kwa wananchi wa Angola.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud