Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamati ya UM yaitaka Djibouti kuzuia ukatili dhidi ya wanawake

Kamati ya UM yaitaka Djibouti kuzuia ukatili dhidi ya wanawake

Kamati ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa imeitaka serikali ya taifa la Djibouti kutekeleza kikamilifu sheria zinazolenga kuwalinda wanawake dhidi ya ukatili.

Kamati hiyo imesema kuwa wanawake wengi nchini Djibouti ni waathirika wa ukatili wa nyumbani, ukiwemo ubakaji katika ndoa ambao unatambuliwa kuwa hatia nchini humo. Katika kauli zilizotolewa baada ya kuhitimishwa kwa kikao chake cha 109 mjini Geneva, leo Alhamis, kamati hiyo pia imetoa wito kwa serikali ifanye juhudi zaidi ili kutokomeza ukeketaji wa wanawake.

Kamati hiyo pia imetoa wito kwa Djibouti kuondoa marufuku ilowekwa dhidi ya vyombo vya habari vya kimataifa nchini humo, kama njia ya kuendeleza haki ya kujieleza.

Ikiwasilisha ripoti yake kuhusu kutekelezwa kwa vipengee vya Mkataba wa Kimataifa kuhusu haki za umma na za kisiasa, serikali ya Djibouti ilisema idadi ya watu nchini humo ni ndogo mno, na haihitaji kuwepo kwa waandishi habari wa kimataifa.

Bi Margo Waterval kutoka Suriname ni mwanachama wa kamati hiyo ya haki za binadamu

“Kuna hatua nyingi zilizopigwa kuboresha hali Djibouti. Wameweka sheria, wameifanyia marekebisho, lakini bado kuna vya kuhofia. Mojawapo, ni ukatili wa nyumbani, ukiwemo ubakaji katika ndoa. Sheria hiyo inatakiwa kufanyiwa marekebisho, kwani ubakaji katika ndoa siyo hatia nchini Djobuti. Wana sheria zinazojaribu kuwalinda wanawake kutokana na ukatili, lakini utekelezaji wake hautendeki vyema. Tunapoongea kuhusu ukatili dhidi ya wanawake, tunazungumzia pia ukeketaji. Wanatakiwa kuongeza ufahamu ili kukomesha desturi hiyo, kwani sheria pekee haiwezi kuikomesha. Wanatakiwa pia kujenga makazi zaidi kwa wanawake wanaoathiriwa na ukatili wa nyumbani.”

Kamati hiyo pia imeelezea kusikitishwa na ripoti za kuteswa kwa watu walotiwa mbaroni na vyombo vya usalama vya dola, na kutoa wito kwa serikali kulinda haki za binadamu za wafungwa.