Baraza la Usalama lamulika hali nchini Somalia

30 Oktoba 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limefanya kikao kuhusu hali nchini Somalia. Akikihutubia kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu, Jan Eliasson, amesema baada ya ziara yake nchini Somalia, amerudi na hisia za matumaini na kutiwa moyo, lakini pia kuna mengi ya kuhofia. Joshua Mmali na taarifa kamili

TAARIFA YA JOSHUA

Bwana Jan Eliasson, ameliambia Baraza la Usalama kuwa ametiwa moyo na kujitoa kwa serikali ya Somalia na watu wake, pamoja na wadau wa kimataifa kwa ajili ya kuleta amani, umoja, maendeleo na kuendeleza haki za binadamu nchini humo.

Hata hivyo, Bwana Eliasson amesema ziara yake hiyo pia iliibua sababu za kuwa na hofu

“Kama Katibu Mkuu alivyoeleza katika waraka wake kwa Baraza hili leo, na kufuatia yale nilosikia nilipokuwa nchini humo, hali Somalia kwa wakati huu bado ni tete. Kuna matarajio mengi yanayoelekezwa kwa Umoja wa Mataifa. Matokeo ya tathmini ya ujumbe wa Muungano wa Afrika na Umoja wa mataifa ni dhahiri. Baada ya miezi 18 ya kuwatimua Al- Shabaab kutoka miji mikuu, kampeni ya AMISOM imekwama.”

Akiongea baada ya Bwana Eliason, Naibu Waziri Mkuu naWaziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, Fawzia Yusuf Haji Adan ametoa shukrani za dhati kwa Baraza la Usalama, lakini pia ameelezea wasisi wake.

CLIP

“Kwa moyo wa dhati kabisa nashukuru Rais na wajumbe wa baraza mlivyojitoa kusaidia Somalia, hatuna shaka kuwa matamanio yetu ya kuwa na Somalia yenye amani na ustawi yatafikiwa! Maendeleo makubwa yamepatikana Somalia na serikali pamoja na wananchi wamejizatiti kuimarisha ushirikiano na marafiki zetu na jamii ya kimataifa.”