Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mimba za utotoni huathiri afya, elimu na haki za watoto wa kike: UM

Mimba za utotoni huathiri afya, elimu na haki za watoto wa kike: UM

Kila mwaka, watoto milioni 7.3 wa kike chini ya umri wa miaka 18 hushika na kujifungua mimba, imesema ripoti mpya kuhusu hali ya idadi ya watu mwaka 2013, ambayo imetolewa na Shirika la Mfuko wa Idadi ya Watu katika Umoja wa Mataifa, UNFPA.  Taarifa kamili na Assumpta Massoi:

(RIPOTI YA ASSUMPTA)

Ripoti hiyo imesema, milioni mbili kati ya watoto hao milioni 7.3, wana umri usozidi miaka 14, na kwamba watoto hao hukumbana na matatizo ya muda mrefu ya kiafya na kijamii kutokana na mimba hizo, yakiwemo vifo vinavyohusiana na uzazi.

Ripoti hiyo pia inatoa wito wa kubuni mbinu za kina za kukabiliana na changamoto za mimba za utotoni.

Inahimiza uwekezaji zaidi katika elimu ili kuhakikisha watoto wa kike wanaendelea kuwa shuleni, kutokomeza ndoa za utotoni, kubadilisha mitazamo kuhusu majukumu ya kijinsia na usawa wa kijinsia. Pia inapendekeza kuongeza ufikishaji wa huduma za afya ya uzazi kwa watoto walobalehe, zikiwemo kuzuia mimba na kuboresha usaidizi kwa wazazi wa utotoni.

Alanna Armitage ni Mkurugenzi wa afisi ya UNFPA mjini Geneva:

“Mimba za utotoni huathiri afya, elimu na haki za mtoto wa kike. Mtoto wa kike asiye na elimu atakuwa na ugumu kupata ajira na kujijengea maisha bora na familia yake. Msichana anayeshika mimba akiwa na umri wa miaka 14 au chini yake, haki zake zitakuwa zimekiukwa. Kuna wasichana milioni 580 duniani sasa. Ripoti ya mwaka huu inaonyesha kuwa kwa kuwekeza kwa watoto wa kike, kuwapa nguvu, na kulinda haki zao leo, tunaweza kuwasaidia kufikia ndoto zao.”

Ripoti hiyo inatoa mtazamo mpya kuhusu mimba za utotoni, ikiangazia siyo tu tabia za watoto hao kama sababu za mimba hizo, bali pia vitendo vya familia zao, jamii na serikali.