Watetezi wa haki za binadamu kwenye miradi mikubwa huonekana “wapinga serikali”:Mtaalamu maalum

29 Oktoba 2013

Watetezi wa haki za binadamu wanaofanya kazi kwa niaba ya jamii zinazoathiriwa na miradi mikubwa ya maendeleo kila mara hunyanyaswa na hata kupachikwa majina ya wapinga serikali au wapinga maendeleo pindi wanapokuwa wanatekeleza jukumu hilo.

Ni kauli ya Margaret Sekaggya alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York, baada ya kuwasilisha ripoti yake ya mwisho kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Bi.Sekaggya amesema watetezi wa haki za binadamu hulenga kusaidia jamii zinazoathiriwa na miradi kama ile ya barabara, mitambo ya kuzalisha umeme kwa njia ya maji, mabwawa au madini kwa kuwa mara nyingi haki za wananchi hukiukwa lakini wao watetezi wa haki za binadamu wanapojitokeza hukumbwa na matatizo.

(Sauti ya Bi. Sekaggya)

"Watetezi wa haki za binadamu duniani kote ambao wanafuatilia miradi mikubwa ya maendeleo hukumbwa na changamoto kubwa. Hizo ni pamoja na vitisho, manyanyaso, kusakamwa na hata vitisho vya kuuawa, wakati mwingine huuawa na huona vigumu kufuatilia miradi hiyo au kutetea wale wanaofanya kazi kwenye miradi hiyo. Kwa hiyo ripoti hii ni kuhusu mtazamo wa haki za binadamu kama njia bora ya kushughulikia suala hilo.”

Amesema mtazamo wa haki za binadamu inamaanisha kushirikisha watetezi wa haki hizo wakati wa miradi hiyo inapopangwa, inapotekelezwa na wakati wa ufuatiliaji wa ili kuepusha fikra hizo na pia kuondoa mivutano na jamii.