Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahanga wa kimbunga Sandy huko Caribbean wasisahauliwe: UNDP

Wahanga wa kimbunga Sandy huko Caribbean wasisahauliwe: UNDP

Mwaka mmoja baada ya kimbunga Sandy kupiga maeneo ya Caribbean na pwani ya Mashariki ya Marekani, shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa limetaka kutosahauliwa kwa wahanga wa janga hilo hususan wale wa maeneo ya Caribbean.

Heraldo Muñoz, Mkurugenzi wa UNDP ofisi ya Amerika ya Kusini katika tahariri yake iliyochapishwa kwenye mtandao amesema mwaka mmoja baada ya janga hilo bado jitihada za ukarabati zinaendelea na penginepo machungu yaliyowapata wahanga wa mataifa ya Caribbean hayakupatiwa uzito wa kutosha.

Naye Jo Scheuer ambaye ni mratibu wa kukabiliana na majanga katika UNDP amesema kutokana na hali mbaya za kiuchumi na kijamii, wakazi wa nchi zinazoendelea mara nyingi hawajiandai kukabiliana na majanga kama Sandy na kwa bahati mbaya huchukua muda mrefu kujikwamua kutoka madhila yaliyowapata.

Nchini Marekani kumbukumbu zimefanyika maeneo ya Kaskazini-Mashariki ikiwemo jijini New York ambapo kimbunga Sandy kilisababisha hasara ya zaidi ya dola Bilioni 18.