Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yaya Touré balozi mpya wa UNEP

Yaya Touré balozi mpya wa UNEP

Mchezaji wa kimataifa wa Côte d'Ivoire na klabu ya Manchester City ya Uingereza Yaya Touré ametangazwa rasmi kuwa balozi mwema wa Shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP na kuahidi kupambana na biashara haramu ya pembe za ndovu barani Afrika.

Touré ambaye alilazimika kusafiri hadi Nairobi nchini Kenya kuhudhuria hafla ya kutangazwa kuwa balozi wa UNEP, anaungana na mwanamitindo wa Brazil Gisele Bündchen, mcheza filamu wa Marekani Don Cheadle, muigizaji wa kike kutoka China Li Bingbing, mpiga picha raia wa Ufaransa Yann Arthus Bertrand pamoja na mchumi wa India Pavan Sukhdev katika kutoa elimu kwa uma kuhusu athari za uharibifu wa mazingira.

Akiongea baada ya kutawazwa rasmi Touré amesema anasikitika kwamba timu yake ya taifa inaitwa tembo, lakini wanyama hawa wakubwa na wenye neema wamesalia takribani 800 pekee nchini mwake na kuongeza kuwa ujangili ni tishio kubwa kwa Afrika na lazima kuchukua hatua sasa.