WHO yathibitisha mkurupuko wa ugonjwa wa Polio Syria

29 Oktoba 2013

Shirika la Afya Duniani, WHO, limethibitisha kuwepo mkurupuko wa ugonjwa wa kupooza wa polio nchiniSyria, ambao umwaathiri watoto wapatao kumi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Joseph Msami ana taarifa kamili.

(Taarifa ya Joseph Msami)

WHO imesema mkurupuko huo umethibitishwa kwenye eneo la Deir Al Zour mashariki mwa Syria, na umeathiri watoto chini ya umri wa miaka miwili. Visa vingine 12 vya kupooza bado vinachunguzwa ili kuthibitisha ikiwa vimetokana na kirusi cha polio au la.

Hii ni mara ya kwanza kwa ugonjwa wa polio kuthibitishwa nchini Syria katika kipindi cha miaka 15. WHO imesema mamlaka nchini Syria na mashirika ya huduma za kibinadamu yanaendesha kampeni kabambe ya chanjo ili kujaribu kuudhibiti ugonjwa huo usisambae zaidi. Oliver Rosenbauer ni msemaji wa mkakati wa kimataifa wa WHO wa kutokomeza polio.

(Sauti ya Oliver)

Ugonjwa wa polio hutokana na kirusi kinachoambukiza mno, na huwaathiri zaidi watoto wachanga. Kirusi hicho huambukizwa kupitia kwenye chakula kilichochafuliwa, pamoja na maji, na husababisha kupooza, ambako aghalabu huwa ni kwa daima. Njia pekee ya kuzuia polio ni chanjo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter