Baraza Kuu lapitisha azimio kuhusu uondoaji wa vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba

29 Oktoba 2013

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kishindo azimio juu ya umuhimu wa kuondoa vikwazo vya kiuchumi, kibiashara na kifedha vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Cuba. Nchi 188 zimeunga mkono huku Marekani na Israeli zikipinga wakati visiwa vya Marshalls, Micronesia na Palau hazikuonyesha msimamo wowote. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Wajumbe wa baraza hilo kabla ya kupitisha azimio hilo walipatiwa ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ikizungumzia utekelezaji wa azimio la mwaka jana lililotaka nchi wanachama wa Umoja huo pamoja na mashirika kutoa misimamo yao juu ya vikwazo hivyo. Mathalani nchi za Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi zimepinga vikwazo hivyo zikisema ni dhalili na hazivitambui na kwamba vinakwamisha maendeleo ya nchi hiyo huru ikiwemo kudumaza uwezo wa nchi hiyo katika tafiti za kilimo na tiba na hata kushirikiana na nchi zingine.

(Sauti ya Msemaji wa Afrika)

“Afrika inatumai kuwa Marekani kwa mujibu wa malengo na misingi ya Umoja wa Mataifa na maazimio mengine husika ya Umoja wa Mataifa itaondoa vikwazo dhidi ya Cuba. AFrika inaunga mkono rasimu ya azimio lililo mbele yetu kuhusu umuhimu wa kuondoa vikwazo dhidi ya Cuba.”

Kwa mantiki hiyo wajumbe wameazimia kukubali ripoti hiyo ya Katibu Mkuu na kutaka nchi ambazo bado zinatekeleza vikwazo hivyo kuvitupilia mbali huku wakiamua kujumuisha katika mkutano wa 69 wa baraza hilo ajenda ya muda kuhusu umuhimu wa kuondoa vikwazo dhidi ya Cuba.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter