Watoto wa kike hawaendi shule kila mwezi kwa kukosa vifaa vya kujisafi: Mtaalamu huru

28 Oktoba 2013

Kamati za Baraza kuu la Umoja wa Mataifa zimekuwa na vikao vyake mjini New York siku ya Jumatatu ambapo miongoni mwao ni ile ya Tatu inayohusika na undelezaji na ulinzi wa haki za binadamu iliyohusisha wataalamu maalum kuwasilisha ripoti zao za mwaka.

Catarina de Albuquerque alikuwa mmoja wao ambaye ripoti yake iligusia haki ya kupata maji safi na salama, suala la majitaka na pia kujisafi ambapo wakati wa mjadala aliulizwa mambo ya kipekee aliyoshuhudia wakati wa uandishi wa ripoti yake, na alilotaja ni pamoja na changamoto wanazopata watoto wa kike na wanawake kujisafi kila mwezi.

(Sauti ya Catarina)

Wakati wa ziara zangu hupanga kukutana na watoto wa kike, huwa natembelea shule nazungumza na wasichana na wakina mama ambao hunieleza kuwa watoto wao wa kike pindi tu wakibalehe, hubaki nyumbani siku tano kila mwezi kwa sababu hawana vifaa vya kujisafi. Kwa hiyo wanakosa shule kwa jambo ambalo hatuwezi kulifikiria. Kwa hiyo ni lazima suala hili lijumuishwe kwenye ajenda ya baada ya mwaka 2015.”

Bi. Albuquerque ameonya kuwa hiyo ni haki ya msingi na iwapo suala hilo lililojificha halitazingatiwa kwenye ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015, watoto wengi wa kike watakosa shule na hivyo matarajio ya kufikia lengo la elimu kwa wote yataponyoka.

(Sauti ya Catarina)

“Katika kila lengo tunaloweka, iwapo hatutaweka nia ya dhati duniani kuondoka ukosefu wa usawa, linapokuja suala la maji na usafi kuna tafiti zinazoeleza bayana kuwa bila kulenga wale walio pembezoni au waliotengwa, malengo ya dunia hayatafikiwa! Kwa hiyo swali langu ni kwamba tunamaanisha au hatumaanishi? Je tunataka lengo la kila mtu kupata huduma hiyo ifikapo mwaka 2030au 2040? Kama ndio basi hatuwezi kufumbia macho suala la kutokomeza ukosefu wa usawa. Lazima tuipatie kipaumbele na ni lazima kuazimia kuondoka na mambo hayo.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter