Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano kuhusu zao la mpunga lataka uwekezaji zaidi Afrika

Kongamano kuhusu zao la mpunga lataka uwekezaji zaidi Afrika

Kongamano kubwa zaidi barani Afrika juu ya zao la mpunga likihusisha wataalamu, watunga sera na wawakilishi wa wakulima limemalizika huko Cameroon na kutaka Shirika la Chakula na kilimo duniani, FAO kuchochea uwekezaji zaidi unaonufaisha wakulima wadogo. Taarifa zaidi na George Njogopa.

(Ripoti ya George)

Kongamano hilo la Tatu limehudhuriwa na zaidi ya wajumbe 650 kutoka nchi 60, 35 kati yao zikiwa ni za Afrika liliandaliwa na kituo cha mpunga barani Afrika na FAO. Washiriki wameazimia kuongezwa kwa uwekezaji katika kilimo cha mpunga barani Afrika kwa kutumia mbinu za kisasa bila kupokonya haki za wakulima wadogo na wakati huo huo kuinua vipato vyao.

Halikadhalika wametaka kuimarishwa kwa vyama vya wakulima ili waweze kupata thamani ya mazao yao na kuchochea ubia kati ya sekta ya umma na ile binafsi kwenye kilimo cha mpunga.

Akingumza kwenye kongamano hilo, Mkurugenzi msadizi wa FAO anayehusika na ulinzi wa walaji Ren Wang amesema shirika lake limejizatiti kusaidia wakulima wadogo wa mpunga barani Afrika.

AFrika inatarajiwa kuzalisha tani Milioni 27.2 za mpunga mwaka huu, ikiwa ni ongezeko kwa asilimia Mbili ikilinganishwa na mwaka jana huku ikiendelea kupunguza utegemezi kwa zao hilo.