Askari wa Tanzania auawa DR Congo; Ban ashutumu vikali

28 Oktoba 2013

Askari mmoja wa Tanzania aliyekuwa akihudumu kwenye kikosi cha mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko DR Congo, MONUSCO ameuawa.

Ripoti hizo ni kwa mujibu wa Msemaji wa Umoja wa Mataifa ambaye katika taarifa yake ya Jumapili kwa waandishi wa habari amemkariri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon akilaani vikali mauaji hayo yaliyotokea wakati waasi wa M23 waliposhambulia walinda amani hao wa MONUSCO ambao walikuwa wakisaidia jeshi la DR Congo, FARDC kulinda raia huko Kiwanja-Rutshruru, kilometa 25 kaskazini mwa Goma.

Ban ametuma rambirambi kwa familia ya askari huyo pamoja na serikali ya Tanzania huku akisema kuwa Umoja wa Mataifa umejizatiti kuchuka hatua zote muhimu kwa mujibu wa azimio namba 2098 la Baraza la usalama kuhusu kulinda raia Mashariki mwa DR Congo.