Vikosi vya serikali na waasi wa M23 wanapambana huko Goma: Baraza la usalama lataka uchunguzi

25 Oktoba 2013

Mapema hii leo huko Goma, Mashariki mwa DR Congo kumeibuka mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23, mapambano yanayoripotiwa kuhusisha matumizi ya silaha nzito ikiwemo makombora. Msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nesirky amewaambia waandishi wa habari kuwa mapigano bado yanaendelea huko Kibaya kwenye viunga vya mji wa Kibumba kilometa 15 kutoka Goma. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu DR Congo, MINUSCO umesema waasi wa M23 wanarusha mashambulizi kutoka mlima Hehu, Kitoma na Bizuru na kwamba kutokana na mapigano hayo hadi asubuhi raia wapatao Elfu Tano walishavuka mpaka na kuingiaRwanda. Tayari MONUSCO imefanya uchunguzi kwa njia ya anga na imetaka kikundi cha pamoja cha kuchunguza maeneo ya mpakani kufuatilia ripoti ya kwamba kombora limetua upande waRwandakwenye eneo la Kageyo wakati huu ambapo inafuatilia kwa kina hali hiyo. Wakati huo huo wajumbe wa Baraza la Usalama wamezungumzia tukio hilo ambapo katika taarifa yao kupitia Rais wa sasa Balozi Agshin Mehdiyev  kutoka Azerbajian, wamesema wanasikitishwa na hali ya kibinadamu na wametaka uchunguzi ufanyike.

 “Wameeleza wasiwasi wao juu ya madhara ya kibinadamu yatokanayo na mapigano hayo. Wajumbe wa baraza wametaka kundi la pamoja la uchunguzi mipakani lichunguze ripoti ya kwamba kombora kutua Rwanda. Wametaka pande zote kujizuia ili kuepusha mapigano zaidi. Halikadhalika wamesisitiza tena kuunga mkono suluhu la kisiasa kwenye  mzozo huo na kwa mantiki hiyo wanaunga mkono mashauriano ya Kampala.”