Takriban watu milioni 2.5 hawajaweza kufikiwa na misaada Syria: OCHA

25 Oktoba 2013

Mratibu Mkuu wa Misaada ya Kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, Valerie Amos, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na mashirika ya kibinadamu kuwafikishia misaada watu waloathiriwa na mzozo wa Syria, bado misaada hiyo inayotolewa ni haba mno, na haiwezi kukidhi mahitaji makubwa yaliyopo.

Bi Amos amesema, miezi mitatu tangu alipolihutubia baraza hilo mara ya mwisho, bado hawajaweza kuwafikishia misaada zaidi ya takribani watu milioni 2.5, akiongeza kuwa wengi wao hawajawahi kufikiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja.

“Ni mashirika 15 tu ya kimataifa ya misaada ambayo yameruhusiwa kutoa huduma nchini Syria, na yanakabiliana na vizuizi yanapojaribu kuweka vituo vya kitaifa.

Tumeweza kufikia maeneo fulani, lakini udhibiti wa mengine haufahamiki, na ni vigumu mno kuyafikia. Ningependa kusisitiza kuwa, bila shinikizo endelevu kutoka kwa Baraza hili dhidi ya serikali na makundi ya upinzani, itakuwa vigumu kutimiza lolote. Tunahitaji pia ufadhili zaidi.”

Wakati huo huo, Bi Amos ameongeza kuwa utekaji nyara wa wahudumu wa kibinadamu unazidi kuwa jambo la kawaida, kama ilivyo kuvizia na kupora malori ya misaada.