Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia wa Madagascar wahimizwa kudumisha amani wanapohitimisha uchaguzi

Raia wa Madagascar wahimizwa kudumisha amani wanapohitimisha uchaguzi

Wananchi wa Madagascar wamejitokeza kwa wingi leo kupiga kura kumchagua rais mpya, kwa mara ya kwanza tangu kupinduliwa utaratibu wa kikatiba nchini humo zaidi ya miaka mine ilopita. Jason Nyakundi ya na taarifa kamili:

TAARIFA YA JASON

Raia wa Madagascar wamekuwa wakipanga foleni ndefu kumchagua rais mpya kwa mara ya kwanza tangu alipopinduliwa Rais Marc Ravalomanana mapema mwaka 2009.

Uchaguzi huo ambao umeripotiwa kuendeshwa kwa njia ya amani, unaonekana kutoa fursa muhimu kwa taifa hilo ambalo limekuwa katika utata wa kisiasa kujikwamua tena.

Fatma Samoura ambaye ni Mratibu Mkazi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo katika Umoja wa Mataifa, UNDP nchini Madagascar, amesema uchaguzi huo pia unatoa matumaini kwa watu wa Madagascar.

(SAUTI YA FATMA SAMOURA)

“Uchaguzi huu unaashiria matumaini kwa watu wa Madagascar kwa sababu baada ya miaka minne ya mzozo nchi hii imeshuhudia kudorora kwa ustawi wa jamii watu wa Madagascar wameonyesha uwezo wao wa kupiga kura kwa njia ya amani na matumaini ni kwamba watachagua rais ambaye ataweza kukabiliana na umaskini ulioko nchini”

Kuna wagombea thelathini na watatu wa kiti cha urais kwa ujumla kwa, na matokeo ya uchaguzi huo yanatarajiwa katika kipindi cha siku kumi zijazo. Umoja wa Mataifa unatarajia kuwa raia wa Madagascar watadumisha amani hiyo wakati wa uchaguzi hadi na baada ya matokeo kutangazwa.