Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto bado watumiwa vitani DRC

Watoto bado watumiwa vitani DRC

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto katika maeneo yenye migogoro Leila Zerrougui amesikitishwa na matokeo ya utafifi uliotolewa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Jamhuri ya Kidemokrsia ya Kongo, DRC,MONUSCO unaoonyesha kwamba vitendo vya watoto kuhusihwa katika vita na vikundi vyenye silaha nchini humo ni mfumo endelevu.

Grace Kaneiya na melezo zaidi:

Leila Zerrougui amesema kuwa mwenondo wa kuwatumia watoto kwenye mizozo ya vita ni jambo lisilokubalika na linakwenda kinyume na sheria za kimataifa na hivyo  amezikata pande zinazohusika na hali hiyo kuacha mara moja .

Ameeleza kuwa pamoja na kwamba serikali ya Congo imepiga hatua kubwa kwa kuwalinda watoto walioathirika na mapigano lakini inapaswa kwenda mbele zaidi kuhakikisha kwamba wahusika wa matukio ya kuwatumikisha watoto wanachukuliwa hatua kali.

Ripoti hiyo ya MONUSCO  imesema kuwa watoto wengi huajiriwa na makundi ya wanamgambo yaliyoweka kambi katika eneo la Mashariki mwa Congo na kwamba katika uchunguzi wake iliofanya kati ya January 2012 na August 2013 ilibaini kesi zaidi ya 1,000 za kutumika watoto kwenye shughuli za kivita.

Baadhi ya makundi ambayo yanadaiwa kuwaajiri watoto hao ni pamoja na kundi la M 23, Forces démocratiques de libération du Rwanda (FDLR) na Nyatura. Watoto wengi wanaochukuliwa na makundi hayo ni wale wenye umri chini ya miaka 15 na katika baadhi ya maeneo imebainika umri wa watoto hao ulikuwa mdogo usiozidi hata miaka 10.