Kumekosekana chombo cha kumulika maslahi ya wahamiaji:Crépeau

25 Oktoba 2013

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa juu ya haki za wahamiaji François Crépeau ameonya juu ya kukosekana kwa chombo maalumu ndani ya Umoja huo ama kwingineko kwa ajili ya kuangazia maslahi ya wahamiaji akisema kuwa hali hiyo ni hatari kubwa.

Katika ripoti yake aliyoiwasilisha mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mtaalamu huyo amesema kukosekana kwa uwazi wa uwajibikaji juu ya masuala ya wahamiaji, kunatoa taswira mbaya juu ya haki zao za msingi.

Amependekeza haja ya kuwepo kwa chombo maalumu ndani ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kushughulia  haki na maslahi ya wahamiaji kwani hali inayojitokeza sasa inakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu.