UM Tanzania waeleza jinsi miradi ya vijijini ilivyoboresha maisha

24 Oktoba 2013

Miradi tunayotekeleza vijijini nchini Tanzania imekuwa na mafanikio makubwa na imedhihirisha kuwa msingi wa maendeleo ni vijijini kwani zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wanaishi huko. Ni kauli ya  Mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Alberic Kacou aliyotoa kwenye mahojiano maalum na idhaa hii wakati wa maadhimisho ya wiki ya Umoja wa Mataifa. Amesema miradi hiyo imenufaisha watu wengi akitolea mfano mradi wa kunawa mikono kwa maji na sabuni ambao ulitekelezwa ukiwa ni kampeni ya dunia ya kunawa mikono kuepusha maradhi.

 (Sauti Alberic)

 “Kwa mwaka uliopita tumeweza kufikia takribani watoto Elfu Arobaini na Tisa kwenye zaidi ya shule 63.Watoto hao walipatiwa mbinu rahisi ya kuwawezesha watoto; wa  kike na wa kiume kunawa mikono huko Tanzania bara na Zanzibar. Waliboresha afya zao na masomo pia! Ni kwamba unavyoelimisha watoto, ndivyo nao wanaelimisha wazazi, Zaidi ya watu Milioni Tatu walifikiwa na ujumbe huo wa kujisafi, wakizingatia ujumbe rahisi tu wa kunawa mikono kwa kutumia sabuni ikiwa ni sehemu ya kampeni ya dunia ya kunawa mikono.”

Bwana Kacou akagusia pia mradi  uliotokomeza mila potofu ya ukeketaji watoto wa kike, FGM kwa kuweka mbinu mbadala ya watoto wa kike kuzingatia mila bila kupata madhara ya kiafya.

(Sauti ya Alberic)

“Mwaka 2012 tulishuhudia watoto wa kike 375 ambayo ni idadi kubwa zaidi kushiriki kile tunachokiita mbinu mbadala ya kuwa mtu mzima! Hii ina maana mbinu hiyo inawezesha jamii kuhifadhi mila yao ya kufunda watoto bila mila potofu ya ukeketaji.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter