Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo za dharura zapangwa dhidi ya uwezekano wa kuwepo mkurupuko wa Polio Syria

Chanjo za dharura zapangwa dhidi ya uwezekano wa kuwepo mkurupuko wa Polio Syria

Tangu mkakati wa kimataifa wa kutokomeza polio ulipozinduliwa mnamo mwaka 1988, idadi ya visa vya ugonjwa huo wa kupooza imepungua kwa asilimia 99.

Kwa sasa, kuna nchi tatu tu ambazo bado zina ugonjwa huo wa polio, ambazo ni Nigeria, Pakistan na Afghanistan. Wataalamu wanatumai kuwa katika miaka michache ijayo, ugonjwa huo utakuwa umetokomezwa kabisa.

Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani, WHO lina hofu kuwa huenda kuna mkurupuko wa ugonjwa huo nchini Syria, ambao utakuwa ni wa kwanza kuripotiwa nchini humo tangu mwaka 1999, na kwamba huenda ukasambaa kwenye ukanda mzima na kuwa mgumu kudhibitiwa kwa sababu ya machafuko yaliyopo sasa.

Oliver Rosenbauer ni msemaji wa mkakati wa kimataifa wa kutokomeza polio

SAUTI YA Oliver Rosenbauer

“Lengo ni kuhakikisha utoaji wa chanjo unaanza kabla hata mwisho wa mwezi huu, mapema wiki ijayo. Lakini baada ya hapo, kwani eneo lote linakabiliwa na hatari ya kuathiriwa kwa kuwa polio ni ugonjwa wa kuambukiza unaosambaa watu wanapotoka sehemu moja hadi nyingine, mpango huo wa kukabiliana nao unapaswa kupanuliwa kwa nchi nzima na hata kwa nchi jirani, kampeni za chanjo zitafanyika. Kwa hiyo, tunapanga kuaza kampeni hiyo ya kina kwa nchi saba za ukanda mzima mapema mwezi Novemba, na itaendelea labda kwa muda wa miezi sita.”