Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali tambueni jukumu la malezi linalofanywa na wanawake

Serikali tambueni jukumu la malezi linalofanywa na wanawake

Imeelezwa kuwa majukumu yanayofanywa na wanawake majumbani bila malipo yoyote kama vile kupika, usafi malezi ya watoto na hata watu wazima yamekuwa yakiwaengua wanawake katika mfumo wa kijamii pindi yanapokuwa hayatambuliwi. Kauli hiyo ni ya mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu umaskini wa kupindukia Magdalena Sepúlveda ambaye amesema kuwa malezi yanapaswa kuwa jukumu la pamoja la jamii badala ya kuachiwa wanawake pekee.

(Sauti ya Sepulveda)

Siku hizi wanawake hufanya kazi saa nyingi zaidi kuliko wanaume tukizingatia kazi wanazofanya bila malipo, ni kumaanisha majukumu kama kutayarisha chakula, kuhudumia watu wenye ulemavu na watoto na hata watu wazima ama wazee, na mara nyingi sera za umma hazitambui kazi hizo.

Ametaka serikali kutambua jukumu hilo la mwanamke kama suala la msingi la haki ya binadamu kwani kazi hiyo isiyo na malipo ni msingi wa jamii zote duniani na ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo.