Leo ni siku ya Umoja wa Mataifa: Ban ataka ushirikiano zaidi wa kimataifa

24 Oktoba 2013

Siku ya Umoja wa Mataifa leo 24 Oktoba ambapo kauli mbali mbali zimetolewa kukumbusha jukumu la chombo hicho adhimu chenye wanachama 193. Ripoti ya Assumpta Massoi inafafanua zaidi.

 (Taarifa ya Assumpta)

 John Ashe, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika ujumbe wake amesema wakati huu ambapo dunia inahaha kukabiliana na migogoro maeneo mbali mbali duniani,  bila kusahau  uharibifu wa mazingira, shida za kiuchumi na kijamii, Umoja wa Mataifa ni fursa kwa wanachama kutumia uwezo wao kukabiliana na majanga hayo.

Amesema watu Bilioni Moja bado wanaishi kifukara na changamoto zinazidi kila uchao hivyo juhudi za pamoja zahitajika. Naye Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema siku ya leo ni fursa kwa kila mmoja kutathmini kile anaweza kufanya ili dunia iwe pahala bora zaidi wakati huu ambapo kuna changamoto mbali mbali huku ile ya mzozo wa Syria ikisalia kuwa changamoto kubwa.  Amesema mamilioni ya watu duniani bado wanategemea misaada ya kibinadamu huku wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la kupinga silaha za kemikali, OPCW wakifanya kazi bega kwa bega nchini Syria kutokomeza shehena za silaha za kemikali nchini humo.

Katibu Mkuu amesema mwaka huu umeshuhudia nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kushirikiana kutafutia suluhu mizozo, masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu na hata mazingira na hivyo ni matumaini yake kuwa umoja ni nguvu na kwa kuendelea kushirikiana changamoto nyingi zinaweza kukabiliwa.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter