Mizozo inapoaathiri maendeleo, fursa za ukuaji huwepo pia: UNDP

23 Oktoba 2013

Licha ya hatua zilizopigwa katika kuzuia migogoro na majanga mwaka ulopita, nchi nyingi bado zinakumbana na migogoro ya mara kwa mara na aghalabu husalia kwenye lindi la umaskini, imesema ripoti mpya ya Shirika la Mpango wa Maendeleo, UNDP.

Ripoti hiyo ambayo imetolewa wiki hii, inabainisha hatua za ufanisi zilizopigwa na UNDP katika kuzuia na kukabiliana na migogoro na majanga mnamo mwaka 2012. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Ofisi ya Kuzuia Migogoro na Ukwamuaji, Jordan Ryan, maeneo mengi duniani ambako migogoro iliongezeka mnamo mwaka 2012 yalishuhudia mkwamo wa uwekezaji wa maendeleo na mateso kwa wanadamu, hususan katika jamii ambazo ni hafifu na hazina uwezo wa kuhimili athari za mizozo hiyo.

Ripoti hiyo imetaja maeneo ya Kusini mwa Amerika na Karibea, ambako viwango vya juu vya uhalifu na machafuko uongeza umaskini, pamoja na Syria kunakoendelea mapigano na matatizo ya kibinadamu, na Ufilipino ambako kimbuga Bopha kiliwaua zaidi ya watu elfu moja na kuwalazimu mamia ya maelfu wengine kuhama makwao. Msimamizi wa UNDP, Helen Clark, amesema migogoro na majanga haya huzuia maendeleo na kuongeza pengo la kiuchumi, pamoja na kuzuia juhudi za kuwakwamua watu kutoka katika umaskini.

Hata hivyo, ripoti hiyo imetaja maeneo ambako ufanisi ulipatikana pia, kama vile Guatemala, ambako haki imepatikana kwa waathiriwa wa ukiukwaji wa haki za binadamu, na tathmini ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwa uwezekano wa majanga Kyrgyzstan.