Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miradi isiyoharibu mazingira ni gharama lakini ni endelevu: Ban

Miradi isiyoharibu mazingira ni gharama lakini ni endelevu: Ban

Uchangiaji fedha kwa ajili ya miradi inayojali mazingira ni kitovu cha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon wakati akifungua mkutano kuhusu uchangishaji fedha kwa miradi ya aina hiyo huko Copenhagen,Denmark.  Ban amesema mara nyingi serikali au wawekezaji huona ni gharama kubwa kuwekeza katika miradi inayojali mazingira lakini miradi ya namna hiyo ina faida ya muda mrefu na endelevu.

Amesema huu ni wakati wa kutumia fursa ya sasa ambayo ameiita ya kihistoria kwani mwishoni mwa mwaka 2015 dunia imeridhia kuwa na mfumo mpya wa maendeleo endelevu na makubaliano ya kisheria kuhusu mabadiliko ya tabia nchi. Amesema kuna mambo ya kuzingatia…

“Mosi fedha za umma kuwekezwa katika miradi inayojali mazingira, miradi ambayo amesema inahitaji mitaji mikubwa lakini ukata usiwe kikwazo kwani faida ya baadaye ni kubwa. Miradi ya nishati salama inaweza kutumika kwenye zahanati vijjijini, shuleni na hata biashara ndogondogo. Pili uwekezaji binafsi kwenye sekta ya nishati ambao ni muhimu ili kukidhi mahitaji  ya nishati kwenye nchi zinazoendelea, uwekezaji ambao unaweza kuchochewa na uwekezaji bora wa fedha za umma kwenye miradi ya aina hiyo. Tatu mfuko maalum wa kuchangia miradi inayojali mazingira. Hivi sasa hauna fedha ni vyema uanze kazi mapema iwezekanavyo.”

Katibu Mkuu ameonya kuwa kadri ambavyo nchi zinachelewa kuchukua hatua stahiki, ndivyo madhara ya mazingira ya kijamii, kiuchumi na kimazingira yanavyozidi kuongezeka.