Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchakato wa UNICEF waendeleza elimu ya watoto wa kike Niger

Mchakato wa UNICEF waendeleza elimu ya watoto wa kike Niger

Katika eneo hili la kusini mwa Niger, elimu ya watoto wa kike bado inapata pingamizi kutokana na shinikizo la itikadi za kitamaduni. Asilimia 36 ya wasichana nchini humo huingia ndoa za utotoni kabla ya umri wa miaka 15.

Katika kujaribu kupunguza pengo lililopo kati ya watoto wa kike na watot wa kiume wanaokwenda shule, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limekuwa likiendeleza mchakato wa shule zinazojali na kuzingatia maslahi ya watoto, ambao unawapa moyo watoto kwenda shule, hususan wale wa kike.

Katika shule 1,000 nchini Niger, ikiwemo hii ya msingi iitwayo Saran Maradi, usawa karibu unatimia

SOUNDBITE (FRENCH) Maman Boukar Kollimi, Regional Director of National Education in Maradi:

“Hii ni shule ambayo inazingatia vipaumbele kadhaa, yakiwemo mazingira- mazingira safi, yenye kivuli, vyoo na sehemu za maji. Pia ni shule inayoendeleza usawa- watoto wa kike wanapewa fursa sawa na watoto wa kiume kwenda shule. Ni shule yenye uhaba wa vifaa, na walimu wamepata mafunzo kitaaluma. Pia, ni shule ambayo inajumuisha jamii katika kila kitu tunachofanya. Ikiwa wadau hawa wote wanachagizwa, tutakuwa na shule yenye mazingira bora kwa watoto.”

Katika kijiji hiki, ingawa wanawake wachache wamepata nafasi ya kwenda shule, wote wamewapeleka watoto wao wa kike shuleni, na wanazingatia kwa umakini elimu yao

SOUNDBITE (Haussa) Tsayba Laoualy, Parent:

"Asubuhi, sisi wanawake huwaosha, kuwavalisha nguo na kuwapeleka shule. Pia tunahakikisha kuwa wanasoma masomo yao. Kila mtu anapaswa kufuatilia elimu ya mwanae.”

Mamlaka za shule pia zimeweka kamati ya kuhakikisha ujumuishaji wa jamii.

SOUNDBITE (Haussa) Illa Laoualy, Secretary of Saran Maradi School Management Committee:

"Tunatoa maji safi ya kunywa shuleni. Tunajenga madarasa kutumia nyasi, na pia tunahakikisha watoto wanahudhuria masomo yao. Ikiwa wanafunzi hawaji shule, tunathibitisha sababu yao kutokuja. Akiwa kaumwa, tunampeleka kwenye kituo cha afya ikiwezekana.”

Hata hivyo, shule hii yenye kiwango hiki cha uzuri haina bwawa la maji. Haina pia madarasa ya kutosha yalojengwa kwa matofali, na kila mwaka, madarasa yalojengwa kwa nyasi huteketea kwa moto. Hali hii inawavunja moyo wazazi na watoto.

Mfumo wa shule inayomjali mtoto umekuwepo kwa kipindi cha miaka mitano ilopita, lakini uhaba wa ufadhili umesababisha ukosefu wa mahitaji mengi ya kimsingi.

Wakati huu, shule za UNICEF zinazoangazia maslahi ya watoto zinakidhi mahitaji ya asilimia saba tu ya watoto wote milioni mbili nchini Niger. Kuna kazi nyingi ya kufanya, lakini hakuna rasilmali za kutosha kuwafikia wote wenye mahitaji.