Mamia ya wasudan kusini warejea Juba: IOM

22 Oktoba 2013

Jahazi lililokuwa limechukua raia 856 wa Sudan Kusini waliokuwa wakiishi Sudan limetia nanga huko Juba na hivyo kuhitimisha safari ya abiria hao ya siku 17 iliyoanzia mji wa Renk wa jimbo la Upper Nile, kaskazini mwa nchi hiyo.

Kwa miaka kadhaa sasa mpango wa wananchi hao kurejea Sudan Kusini ulikuwa unakwama kwenye mpaka wa kaskazini huko Renk ambapo hata baada ya kuvuka, matarajio ya kuendelea na safari yalikwamishwa na mambo mbali mbali ikiwemo miundombinu duni na ukosefu wa fedha.

Msemaji wa IOM Jumbe Omari Jumbe amesema kupitia mpango wa usaidizi wa kurejea nyumbani uitwao OTA, IOM kuanzia mwaka huu limeweza kusaidia wasudan kusini zaidi ya Elfu Sita.

Amesema zoezi la utambuzi lililofanyika katikati ya mwaka huu huko Renk lilibaini kuwepo kwa watu Elfu Tatu waliokwama eneo hilo wakisubiri kuelekea Sudan Kusini.

Amesema baada ya kukamilika kwa msafara huo hadi Juba ambako raia wengi walisema ndio mwisho wao wa safari na wale waliotaka kusonga zaidi walipatiwa usaidizi, IOM inaendelea na mipango ili kuwepo kwa jahazi lingine kwa msafara mwingine kutoka Renk, wiki chache zijazo.