Baraza la Usalama lakutana kuhusu suala la Palestina na amani Mashariki ya Kati

22 Oktoba 2013

  

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekutana kujadilia suala la Palestina na amani Mashariki ya Kati, wakati ambapo harakati za upatanishi na kusaka amani zimeshika kasi.  Joshua Mmali na taarifa kamili(TAARIFA YA JOSHUA MMALI)

Mkutano wa leo wa Baraza la Usalama umehudhuriwa pia na  wawakilishi wa nchi mbali mbali, zikiwemo zile za eneo la Mashariki ya Kati. Baraza hilo limehutubiwa na Mkuu wa masuala ya kisiasa katika Umoja wa Mataifa, Jeffrey Feltman, ambaye amesema Baraza hilo linakutana wakati wa kuongezeka shughuli za mazungumzo ya amani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Kuhusu Syria, Bwana Feltman amesema ni muhimu kuendeleza mipango ya kongamano kuhusu taifa hilo kati mwa mwezi Novemba, ambalo amesema litalenga kuzisaidia pande zinazozozana Syria kuzindua harakati za kisiasa ambazo zitasaidia kuleta amani ya kudumu.

Kuhusu suala la harakati za amani Mashariki ya Kati, Bwana Feltman amesema kuna haja ya kubadili misimamo kuhusu jinsi ya kukabiliana na suala hilo la amani, na kutafuta suluhu la dharura kwa miongo ya mizozo kati ya Israel na Palestina.

“Tufanye kila tuwezalo kuudakia mlango wa fursa iliopo sasa. Hilo litawafaa watu wa Palestina na Israel, na ukanda mzima. Baada ya miaka 20 ya mazungumzo na vizuizi vingi, hatuhitaji mazungumzo ya muda mrefu. Tunachohitaji sisi na pande husika ni maamuzi. Maamuzi bora na viongozi ambao wanajitoa kwa kuleta suluhu la kisiasa.”