Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rangi za mapambo zenye madini ya risasi zahatarisha maisha ya watoto na wajawazito: UNEP

Rangi za mapambo zenye madini ya risasi zahatarisha maisha ya watoto na wajawazito: UNEP

Zaidi ya miaka 90 tangu mjumuiko wa mataifa kutoa wito wa kupiga marufuku matumizi ya madini ya risasi kwenye rangi za mapambo na licha ya kuwepo kwa njia nyingine za kuboresha rangi hizo bila kutumia risasi, bado yaelezwa kuwa madini hiyo yatumika.

Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP linasema kitendo hicho kinaweka hatarini afya za watoto na wajawazito hususan kwenye nchi zinazoendelea kwani wanakabiliana na rangi zenye kiwango kikubwa cha madini hayo ambayo si salama.

Utafiti wa UNEP wa rangi za mapambo kwenye nchi Tisa zikiwemo Ethiopia na Ghana umeonyesha kuwa rangi nyingi hazikidhi viwango vya usalama kwani zina kiwango kikubwa cha madini ya risasi ikilinganishwa na rangi zinazopatikana kwenye nchi zilizoendelea.