UM kuendeleza usaidizi kwa NEPAD na mchakato wa APRM: Ban

21 Oktoba 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amepongeza mpango wa nchi za Afrika wa kujitathmini wenyewe, APRM akisema kuwa mpango huo siyo tu umeimarisha utawala wenye misingi ya kidemokrasia barani humo bali pia umefungua fursa zaidi kwa raia kushiriki kwenye maamuzi yanayowahusu. Bwana Ban amesema hayo katika mjadala maalum uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa ukiwa umeandaliwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya mshauri maalum wa masuala ya Afrika ikiwa ni sehemu ya wiki ya Afrika katika umoja huo.  Amezipongeza nchi 17 za Afrika ambazo zimeshafanya tathmini hiyo na kutoa ripoti zao huku akieleza kuwa…

(Sauti ya Ban)

“Katika baadhi ya maeneo, APRM imefichua vyanzo vya mizozo na kutoa mapendekezo ya jinsi ya kutatua. APRM  imebainisha maeneo kadhaa ambayo nchi za Afrika zinapaswa kuboresha. Imeonyesha umuhimu wa kusimamia vyema maliasili, kuzuia rushwa, kutokomeza chuki dhidi ya wageni na hata ugaidi. Zaidi ya yote, APRM inaonyesha umuhimu wa kupiga vita mapinduzi ya kijeshi na pindi yanapotokea kuchukua hatua stahiki na kulinda misingi.”

Bwana Ban akasema sasa ni wakati wa kuimarisha tunu hiyo muhimu ili nchi nyingi zaidi ziendelee kunufaika na Umoja wa Mataifa uko pamoja na Afrika kuhakikisha mpango wa maendeleo kwa Afrika NEPAD na APRM vinaendelea kustawi.

(Sauti ya Ban)

 “Kile ambacho APRM inafanya kwa utawala bora, NEPAD inafanya kwa maendeleo. Kwa pamoja vinasaidia Afrika kusonga kwenye mwelekeo sahihi wa demokrasia na maendeleo na kunufaisha wananchi wake.”

Nchi za Afrika zilizokwisha kufanya tathmini ni pamoja na Kenya, Tanzania,  Rwanda na Ghana