Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lasikiliza ripoti za ziara ya wanachama kwa Maziwa Makuu

Baraza la Usalama lasikiliza ripoti za ziara ya wanachama kwa Maziwa Makuu

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limesikiliza ripoti mbali mbali kuhusu hali ya amani na usalama kwenye ukanda wa Maziwa Makuu kufuatia ziara ya wanachama wake kwenye ukanda huo hivi karibuni. Joshua Mmali amefuatilia mkutano huo.

 (TAARIFA YA JOSHUA)

Kwanza, wanachama wa Baraza la Usalama, wakiwemo wawakilishi wa kudumu wa Morocco, Rwanda, Uingereza na Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, wametoa ripoti kuhusu ziara yao kwenye nchi za Maziwa Makuu, na kuelezea kuridhishwa kwao na mchango wa Uganda katika kuendeleza harakati za amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, DRC.

Baadaye, Baraza hilo limesikiliza ripoti ya Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu, na Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu DRC, Martin Kobler, ambaye amelihutubia kwa njia ya video kutoka Entebbe, Uganda. Katika hotuba yake, Bwana Kobler amesema waasi wa M23 wameendelea kufanya mashambulizi yanayoulenga ujumbe wa Umoja wa Mataifa, yakiwemo kuzifyatulia risasi ndege za Umoja wa Mataifa. Ameongeza kuwa ili harakati za amani zifanikiwe, wahusika wote wanatakiwa kujitoa na kuelekeza juhudi zao kwenye mkondo wa kusaka amani.

Kurejeshwa kwa mamlaka ya kitaifa mashariki mwa DRC ni bora zaidi kwa ukanda mzima kuliko kuendelea vurugu za kijeshi, mateso ya wanadamu na uporaji wa madini. Hali kama hii siyo rais. Inategemea utashi wa kisiasa wa wahusika kutekeleza mikataba ilyopo.”

Mwingine aliyetoa ripoti kwa Baraza hilo kupitia njia ya video ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu kwenye nchi za Maziwa Makuu, Mary Robinson, kutoka Addis Ababa, Ethiopia.