Kufuatilia uharibifu wa chakula ni muhimu katika kupiga vita njaa: FAO

21 Oktoba 2013

Kufuatilia na kufahamu kiasi cha chakula kinachoharibiwa ni muhimu katika kupunguza tatizo la njaa, pamoja na kuongeza kasi ya kutokomeza njaa duniani, amesema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo, FAO, José Graziano da Silva, wakati wa kongamano la ukuaji wa kimataifa unaojali mazingira mjini Copenhagen, Denmark.

Kwa mujibu wa makadirio ya FAO, thuluthi moja ya chakula kinachozalishwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu, kiasi ambacho nikamatani bilioni 1.3, hupotea au huharibiwa. Kulingana na Bwana da Silva, uharibifu huu ni sawa na dola bilioni 750 kila mwaka.

Bwana da Silva amesema ikiwa uharibifu wa chakula utapunguzwa na kutokomezwa kabisa, kutakuwepo chakula zaidi cha kutosha kuwalisha watu bilioni mbili.

Kongamano hilo la Copenhagen la Oktoba 21-22 linawaleta viongozi wa mashirika mbalimbali pamoja kujadili mikakati ya viwango wastani vya kimataifa vya kupima uharibifu wa chakula.