Tahir yachangia dola Milioni 65 kwa Global Fund

21 Oktoba 2013

Mwenyekiti wa mfuko wa Tahir nchini Indonesia Dk Tahiri ametangaza leo kuwa mfuko wake huo unatoa kiasi cha dola za Marekani milioni 65 kusaidia juhudi zinazoendeshwa na Global Fund za kukabiliana na magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria.

Mchango huo unafungana na ule uliotolewa na wakfu wa Bill & Melinda Gates na hivyo kufanya Global Fund kukusanya jumla ya dola milioni 130 ili kutekeleza miradi yake. George Njogopa na taarifa kamili

(TAARIFA YA GEORGE NJOGOPA)

Kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na mfuko wa Tahir ambacho ni kikubwa zaidi kuwahi kutolewa na taasisi binafsi kutoka katika nchi inayochipukia kiuchumi, kinatazamiwa kutumika kwenye miradi ya uchunguzi wa magonjwa, tiba pamoja na utoaji kinga dhidi ya magonjwa ya Kifua Kikuu, Ukimwi na Malaria.

Magonjwa hayo yanatajwa kuwa tishio kubwa nchini Indonesia na ndiyo yanayoongoza kwa kusababisha vifo vingi.

Kutolewa kwa msaada huo kunakuja katika wakati ambapo fuko hilo la kimataifa yaani Global Fund kilijiandaa na mkutano wake wa nne mwezi utakaofanyika Disemba huko Washington kwa ajili ya kutathmini miradi yake.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Mjini Jarkata, Indonesia Dk Tahir alisema kuwa wakfu wake utafungamana na malengo yanayosimamiwa na Global Fund.

Ufadhili unaotolewa na Global Fund katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita, umewasaidia zaidi ya watu milioni 1.3 nchini Indonesia waliokuwa wakikabiliwa na matatizo ya kifua kikuu. Pia katika kipindi hicho shirika hilo limefaulu kusambaza vyandarua vilivyonyunyuziwa dawa zaidi vinavyokadiriwa kufikia milioni 9.