Uongozi wa wanawake ni muhimu katika kuendeleza amani: UN Women

18 Oktoba 2013

Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Wanawake katika Umoja wa Mataifa, UN Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka, amekaribisha hatua ya Baraza la Usalama kupitisha azimio la kuongeza nafasi za mchango wa wanawake katika kuzuia na kutatua mizozo, pamoja na kuendeleza amani.

Azimio hilo ambalo limepitishwa katika kikao maalum mnamo Oktoba 18, linatoa pia wito wa kuchukuliwa hatua mathubuti za kuongeza idadi ya wanawake katika upatanishi wa amani, na kuboresha jinsi masuala ya jinsia yanavyozingatiwa na taasisi za amani na usalama, likiwemo Baraza la Usalama lenyewe.

Amelishukuru Baraza la Usalama kwa kuonyesha ari yao katika azimio hilo namba 2122, ya kuweka uongozi wa wanawake katikati ya juhudi zote za kutatua mizozo na kuendeleza amani.

Amesema azimio hilo linakabidhi majukumu kwa wote- Baraza la Usalama, Umoja wa Mataifa, mashirika ya kikanda na nchi wanachama- kutoa nafasi na kuongeza viti vya wanawake kwenye meza ya amani.

(Phumzile Mlambo-Ngcuka)

“Nafahamu bila shaka kuwa wanawake wamehitimu ipasavyo kutekeleza majukumu haya, na wapo tayari kuteuliwa kwa ngazi hizo za juu. Ni muhimu wanachama wa Baraza la Usalama waombe maelezo kuhusu mchango wanaotoa wanawake katika kutatua mizozo, na hili limetambuliwa na azimio hili. Kuwajumuisha wanawake tu haitoshi. Wadau wote ni lazima wapate upeo wa kitaaluma kwa masuala ya jinsia"