Ban azungumzia ripoti kuwa Saudi Arabia ‘imekataa’ ujumbe kwenye Baraza la Usalama

18 Oktoba 2013

Bado sijapokea taarifa rasmi kuhusu ripoti za Saudi Arabia kukataa ujumbe usio wa kudumu kwenye baraza la usalama. Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon aliyotoa mchana huu alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusiana na sualahilolililoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari. Bwana Ban amesema ujumbe ndani ya Baraza la Usalama ni uamuzi wa nchi mwanachama hata hivyo akasisitiza:

(Sauti  ya Ban)

“Lakini ningependa kuhadharisha uwa sijapokea tangazo rasmi kuhusu suala hilo. Nazisihi nchi wanachama kushiriki ipasavyo kwenye vyombo vya Umoja wa Mataifa huku zikiimarisha jitihada za kuboresha utendaji wa vyombo hivyo. Halikadhalika tunatarajia kushirikiana kwa karibu na ufalme wa Saudia katika kushughulikia changamoto kadhaa ikiwemo kumaliza vita nchini Syria, kusaidia wapalestina kupata taifa lao na kusaidia kipindi cha mpito nchini Yemen bila kusahau kutoa usaidizi wa kibinadamu kwa watu wote wenye mahitaji, kudhibiti ugaidi na ueneaji wa silaha za nyuklia.”

Bwana Ban akaulizwa iwapo atazungumza na Mfalme waSaudi Arabiakwa njia ya simu.

(Sauti ya Ban)

Nafikiria jinsi ambavyo tutashughulikia suala hili. Nafahamu nchi wanachama mmoja mmoja zinajadili. Nitafuatilia kwa karibu nione uamuzi wao ni upi kuhusu suala hili.”

Jana Alhamisi, Baraza Kuu lilipiga kura kuchagua wajumbe watano wapya wasio wa kudumu ambapo Saudi Arabia ilikuwa miongoni mwa nchi zilizopata theluthi mbili ya kura zinazohitajika na kutangazwa mshindi. Nchi nyingine ni Chile, Lithuania, Nigeria na Chad.