Baraza la Usalama laazimia kutambua umuhimu wa wanawake katika kuendeleza amani

18 Oktoba 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo katika kikao maalumu limepitisha azimio la kuutambua umuhimu wa wanawake katika kuzuia na kutatua mizozo, pamoja na kuendeleza amani. Grace Kaneiya ana ripoti kamili.

(Taarifa ya Grace Kaneiya)

Azimio la kuutambua mchango wa wanawake limepitishwa katika wakati Baraza la Usalama likikutana kujadili suala la wanaw ake, uongozi wa kisheria na mchango wao katika upatikanaji haki wakati wa mpito baada ya mizozo.

Azimio hilo pia linatoa wito wa kuchukuliwa hatua mathubuti za kuongeza idadi ya wanawake katika upatanishi wa amani, na kuboresha jinsi masuala ya jinsia yanavyozingatiwa na taasisi za amani na usalama, likiwemo Baraza la Usalama lenyewe.

Miongoni mwa waliohudhuria kikao cha leo, ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, aliyelisifu azimio hilo

(Sauti ya BAN)

“Uongozi wa kisheria, upatikanaji haki kwa wanawake baada ya mizozo na kuwajumuisha ni vitu vinavyoambatana kwa karibu. Wanawake ni lazima wajumuishwe kwenye kila ngazi ya juhudi za kurejesha uongozi wa kisheria na kujenga upya jamii kupitia mfumo wa haki wakati wa mpito. Mahitaji yao ya usalama na haki ni lazima yazingatiwe. Sauti zao ni lazima zisikike. Haki zao ni lazima zilindwe.”

Mwingine aliyekuwepo kwenye kikao na kulikaribisha azimio hilo ni Mkurugenzi Mkuu wa kitengo cha wanawake, UN WOMEN, Phumzile Mlambo-Ngcuka

(Phumzile Mlambo-Ngcuka)

Nafahamu bila shaka kuwa wanawake wamehitimu ipasavyo kutekeleza majukumu haya, na wapo tayari kuteuliwa kwa ngazi hizo za juu. Ni muhimu wanachama wa Baraza la Usalama waombe maelezo kuhusu mchango wanaotoa wanawake katika kutatua mizozo, na hili limetambuliwa na azimio hili”