Sheria za kutetea watoto bado zina ubaguzi dhidi ya watoto wa kike: Ripoti

18 Oktoba 2013

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kupinga ukatili dhidi ya watoto Marta Santos Pais amesema licha ya serikali kupitisha sera na sheria za kupinga vitendo hivyo, bado kuna ubaguzi wa jinsi ambavyo sheria hizo zinatetea kundi hilo.  Akizungumza katika mahojiano maalum na Radio ya Umoja wa Mataifa kuhusu ripoti aliyowasilisha mbele ya Baraza Kuu wiki hii, Bi. Pais amesema ni nadrasanakuona katika nchi uwepo wa sheria ambazo zinalinda watoto kike sawia na watoto wa kiume. Ametoa mfano wa ndoa za umri mdogo ambazo amesema ni mojawapo ya mfano wa vile ambavyo sheria inawatendea watoto wa kike tofauti na watoto wa kiume. Amesema katika mfumo wa haki, wasichana mara nyingi wanaadhibiwa kwa sababu wanaonekana kuwa na makosa ya kimaadili. Bi. Pais amesema jambo hilo halina ainisho dhahiri na hivyo kuwaweka kwenye hatari ya kuwa jela kwa kipindi kirefu, jambo ambalo halipaswi kuwa hivyo. Mfano mwingine ametaja ni ule wa watoto wa kike kutumbukia katika kazi za majumbani kwa kuwa hawana fursa ya kupata elimu. Hata hivyo ripoti hiyo kuhusu hatua za kudhibiti ukatili dhidi ya watoto imeweka bayana kuwa baadhi ya nchi zimefanya vyema kudhibiti ukatili dhidi ya watoto wote na kwamba sheria ni muhimu ili iwe mwongozo wa kudhibiti vitendo hivyo.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter