Tume ya UM kuhusu Korea Kaskazini kukusanya maoni Uingereza na Marekani

17 Oktoba 2013

Tume ya Umoja wa Mataifa yenye mamlaka ya kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Korea Kaskazini wiki ijayo itakuwa Uingereza na Marekani ambapo watu wenye ushahidi wa ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Korea Kaskazini watatoa ushuhuda wao. Taarifa iliyotolewa leo imesema jopo hilo la watu watatu litakuwa London tarehe 23 na baadaye Washington D.C tarehe 30 na 31 mwezi huu. Wanaotarajiwa kutoa ushuhuda ni pamoja na wananchi ambapo mwenyekiti wa tume hiyo Michael Kirby amesema shughuli hiyo itatoa fursa muhimu ya kupata ushahidi utakaowezesha jumuiya ya kimataifa kutambua hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu huko Korea Kaskazini. Bwana Kirby amesema ijapokuwa hawana mawasiliano ya moja kwa moja na serikali ya Korea Kaskazini, bado wanaweza kukusanya taarifa muhimu kutoka kwa watu ambao wamekuwa jasiri na kujitokeza kutoa simulizi juu ya madhila yaliyowakumbua nchini humo. Kabla ya kwenda Washington D.C jopo hilo litakuwepo New York tarehe 28 na 29 ambapo watakuwa na mazungumzo na maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa na kutoa taarifa ya awali kwa Baraza Kuu.