Leo ni siku ya kutokomeza umaskini duniani

17 Oktoba 2013

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu umaskini Magdalena Sepúlveda, amezitaka nchi kuzitambua na kuthamini kazi za ndani zinazofanywa bila malipo akisema kuwa lazima sasa ziungwe mkono na kutoa usawa kwa wote wanawake na wanaume.

Akizungumza katika siku za kutokomeza umaskini duniani, mjumbe huyo ameonya kuwa kukosekana kwa usawa kwa kazi hizo, kunazidisha kitisho juu ya haki za binadamu.

Wengi wanaamini kwamba shughuli za majumbani kama vile  kuangalia watoto na mapishi ni jukumu la wanawake pekee, jambo ambalo linapingwa vikali na watetezi wa haki za binadamu.

 Mtaalamu huyo amezitaka nchi kote duniani kuchukua hatua maalumu kuondosha kasumba hiyo ambayo inaendelea kuwakandamiza wanawake na hivyo kuwafanya watu wa daraja la chini.

Amezitaka nchi hizo kuweka sera zitakazofafanua bayana kuhusiana na huduma za kijamii na kuongeza umaskini wa dunia hauwezi kuondoka kama wanawake wataendelea kubaguliwa.