Ujumbe wa pamoja wa UM na OPCW unaosimamia Syria waanzishwa rasmi leo

16 Oktoba 2013

Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na shirika la kimataifa la kupinga matumizi ya silaha za kemikali, OPCW umeanzishwa rasmi hii leo tarehe 16 Oktoba kufuatia mashauriano ya karibu kati ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa. Taarifa ya pamoja ya pande mbili hizo iliyotolewa leo mjini New York, imesema kuwa hatua hiyo inanzigatia vipengele vya uamuzi uliochukuliwa na baraza tendaji la OPCW tarehe 27 mwezi uliopita na kufuatia na azimio namba 2118 lililopitishwa na baraza la usalama. Lengo la ujumbe huo ni kukamilisha katika muda unaotakiwa utokomeza wa mpangowa silaha za kemikali nchini Syriakwa njia sahihi na salama. Halikadhalika ujumbe huo utaendeleza kazi iliyokuwa imeanza kufanywa mwanzoni mwa mwezi huu na jopo la pamoja la OPCW na Umoja wa Mataifa nchini Syria. Sambamba na kuanzishwa rasmi kwa ujumbe huo hii leo, OPCW na Umoja wa Mataifa wameanzisha mifuko wa wadhamini kwenye makao makuu ya taasisi hizo mbili. Matukio yote ya leo kuanzia kuanzishwa rasmi kwa ujumbe huo, uteuzi wa mratibu maalum Sigrid Kaag na mifuko ya wadhamini inatokana na mapendekezo ya Katibu mkuu Ban Ki-Moon aliyoandaa kwa mashauriano na Mkurugenzi Mkuu wa OPCW, Ahmet Üzümcü.