Idadi ya watu duniani wanaokosa mlo kwa siku yapungua: FAO

16 Oktoba 2013

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema idadi ya watu wanaoshinda njaa kutwa duniani imepungua lakini bado juhudi zahitajika ili kutokomeza njaa. FAO imesema hata hivyo harakati za kuimarisha lishe bora hazitafanikiwa iwapo hakuna mifumo bora ya uhakika wa chakula na hata ya kupata mlo bora. Ripoti ya Assumpta Massoi inafafanua zaidi.

(Ripoti ya Assumpta)

Idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa kila siku imepungua kutoka Milioni 870 mwaka 2012 hadi Milioni 840 mwaka huu, amesema Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Jose Graziano Da Silva kwenye kilele cha siku ya chakula duniani huko Roma. Amesema kupungua idadi hiyo kunaonyesha matumaini kuwa mifumo sahihi ya uzalishaji, uhifadhi na usambazaji chakula inafanya kazi. Amesema nchi 62 zinazoendelea kati ya 128 zinazofuatiliwa na FAO zimefikia lengo la Milenia la kupunguza njaa, lakini bado kuna kazi kubwa ili kila mtu awe na uhakika wa mlo bora na wa uhakika…

(Sauti ya Graziano)

Naye Mkurugenzi mkuu wa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP, Etharin Cousin ametaka uwekezaji zaidi kwenye lishe kama njia ya kubadilisha kiuchumi maisha ya jamii zote duniani.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ni ajabu zaidi ya Watu Milioni 840 duniani wanashinda na njaa ilhali kuna rasilimali za kutosha duniani. Amesema jibu pekee ni kuhakikisha kila mtu anapata mlo sahihi kwa kuhakikisha kuna mifumo, sera na uwekezaji bora unaoweka fursa ya mazingira bora na watu kuzalisha mazao bora na salama na kufikia watu kwa uhakika.